Aliyekuwa Chifu wa eneo la Raruma, Kaunti ndogo ya Rabai, amewaonya walimu katika eneo la Pwani dhidi ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza kwenye hafla ya kufungua shule mpya ya chekechea huko Raruma Kaunti ndogo ya Rabai, Thomas Chippi alisema kuwa baadhi ya walimu huwatuma wanafunzi kwenda kuwatekea maji na kuwapelekea kwao majumbani kisha baadae kuwarai kufanya tendo la ndoa.

Chippi alisema muhula uliopita alishuhudia zaidi ya wanafunzi wanne wakilazimika kuacha shule kutokana na mimba za mapema ambazo alisema zilichangiwa na tabia mbovu miongoni mwa walimu.

Kulingana na Chippi, mtoto wa kike ndiye anayeathirika zaidi katika maswala ya uhusiano wa kimapenzi na hivyo basi inapaswa atunzwe ili kumuepusha na kutumika vibaya.

Chifu huyo wa zamani alisema baadhi ya walimu hushiriki tendo la ndoa na wanafunzi walio katika madarasa ya chini, jambo ambalo alisema huchangia pakubwa katika kudorora kwa maadili miongoni mwa jamii mbalimbali nchini.

Aidha, alisema kuwa serikali inapaswa kukomesha tabia ya wanafunzi wa kike kwenda kufanyiwa mafunzo ya ziada nyumbani mwa walimu wao.

Chippi aliwataka wanafunzi kutambua kuwa wanaposhiriki tendo la ndoa na walimu wao, hao ndio wanaopoteza zaidi kwani bado wangali wachanga na wana mengi ya kutimiza katika ulimwengu wa sasa.