Walimu wakuu wa shule za msingi wamepinga kanuni mpya zilizobuniwa na Baraza la Mitihani nchini Knec zinazolenga kukabili udanganyifu katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE.
Naibu katibu wa maswala ya nyanjani katika baraza la Knec Mahamud Ibrahim, siku ya Jumanne alilazimika kukatiza hotuba yake alipokuwa akihutubia walimu hao katika kongamano linaloendelea mjini Mombasa baada ya kuzomewa na walimu hao wakuu.
Walimu hao walisema hawako tayari kufanya kazi ya kutahini mtihani huo, huku wakishikilia kuwa hatua ya Knec ya kuwataka kutahini mtihani inalenga kuwatia kwenye mtego wa kulimbikiziwa lawama iwapo kutatokea wizi wa mtihani.
Miongoni mwa masuala yanayozua utata kutokana na kanuni hizo mpya ni kuwataka walimu wakuu kuchukua karatasi za mtihani kutoka katika kituo kikuu cha mtihani na kisha kuziregesha baada ya mtihani huo kukamilika kando na pia kuwa wasimamizi wa mtihani katika shule zao.
Akitangaza kanuni hizo mpya mwezi Mei, Waziri wa Elimu Fred Matiang’i alisema kuwa walimu wakuu watasimamia mtihani katika shule zao ili kupunguza visa vya baadhi ya walimu kushirikiana na wanafunzi kuiba mtihani huo.
Matiang'i alisema hiyo itasaidia kukabili wizi wa mtihani shuleni kwa kuwa kila mwalimu mkuu atahitajika kufafanua iwapo kutatokea kisa chochote cha wizi wa mtihani katika shule yake.
Kongamano la walimu hao ambalo lilianza siku ya Jumamosi, litakamilika siku ya Ijumaa.