Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Shughuli za masomo katika shule nyingi za umma katika kaunti ya Mombasa zimeendelea kutatizika huku walimu wakikataa wito wa rais wa kuwataka kuripoti kazini kwa madai kuwa serikali haina fedha za kuwalipa.

Wakiongozwa na katibu wa chama cha Knut tawi la Kilindini Dan Aloo, walimu wa shule za umma maeneo ya Changamwe, Kaunti ya Mombasa, washiriki maandamano siku ya Jumanne, ili kuishinikiza serikali kuwapa mishahara yao.

“Tunamwomba Rais Uhuru Kenyatta asisikize ushauri potofu kutoka kwa baadhi ya viongozi serikalini na badala yake kuhakikisha kuwa walimu wanapata haki yao kwa mujibu wa sheria kama ilivyo amriwa na mahakama,” alisema Aloo.

Walimu waliingia kwenye mgomo mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya serikali kukiuka agizo la mahakama la kuwapa nyongeza ya mshahara wa kati ya asilimia 50 na 60.

Walimu wamekuwa wakikumbwa na mizozo ya mishahara iliopelekea migomo kwa muda sasa ambapo wanafunzi katika vizazi tofauti wamekuwa wakiathirika na migomo hiyo.