Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa amewasuta viongozi wa Pwani walioasi chama cha ODM.
Jumwa alidai kuwa viongozi hao wameanza kususua baada ya kuchukua hatua ya kujiunga na chama kipya cha Jubilee.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika afisi yake, Jumwa alisema tayari wametayarisha mchakato wa kuwashinikiza viongozi hao kutoendelea kuwa madarakani kutokana na hatua ya kugura chama kilichowaweka katika nyadhifa wanazoshikilia.
Jumwa alitoa mfano wa Gavana wa Kwale Salim Mvurya aliyedai kuwa Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kufanya mazungumzo ya kisiri ya kumnyima tiketi ya kugombea kiti cha ugavana eneo la Kwale.
Alisema hiyo ni ishara tosha kuwa viongozi hao wameanza kuonja sehemu chungu ya chama cha Jubilee.
“Viongozi waliogura ODM wanatafuta tu maneno ya kuharibia viongozi wenzao sifa kwa wakaazi wa Kwale na kisha kuwaharibia kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao,” alisema Jumwa.
Aidha, alisema kuwa kusuasua kwa viongozi hao hakupaswi kuanza sai kwani mwaka ujao ndipo watatambua kweli kuwa mrengo wa Cord ulikuwa umejiandaa kunyakua nafasi zote katika eneo la Pwani.
“Kiti cha urais na naibu wake lazima kiende kwa mrengo wa Cord ambao mara nyingi umekuwa ukidhulumiwa kwenye chaguzi mbalimbali zilizofanyika hapa nchini,” alisema Jumwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wadi ya Ganze Katana Nzaro amewahakikishia wakaazi kuwa chama cha ODM kitachukua nyadhifa za uongozi katika eneo hilo wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
“Endapo wenyeji wataruhusu mgombea wa chama cha Jubilee kuchukua wadhifa wowote eneo hili, basi itakuwa mwanzo wa kujizika tena katika masaibu ya uhaba wa maji na baa la njaa linaloendelea kukumba eneo hili,” alisema Nzaro.