Madiwani wa zamani katika kaunti ya Kisii wameomba wale wote walipanga njama ya kumchafulia jina naibu Gavana wa kaunti hiyo Joash Maangi katika mtandao kujitokeza kuomba msamaha ili kuzuia laana kuwaandama.
Hii ni baada ya picha za Maangi kusambazwa mtandaoni akiwa uchi wa mnyama kwa juma moja lililopita huku washukiwa wawili wakitiwa mbaroni kuhusiana na kisa hicho, na ikidaiwa kuwa kuna mmoja wa mwakilishi wadi katika kaunti hiyo aliyepanga njama hiyo .
Wakizungumza siku ya Jumanne walipomtembelea naibu gavana afisi mwake iliyoko mjini Kisii madiwani hao wa zamani wakiongozwa na Gichana Ong’ondi na Ombasa Tamaro waliomba wale wote waliounda njama hiyo kujitokeza na kuomba msamaha ili laana zisiwaandame
“Wale waliopanga njama hiyo wanafaa kujitokeza wazi waombewe ikiwezekana, maana yale walitekeleza ni kinyume na jamii yetu ya Kisii,” alisema Ong’ondi.
“Hakuna vile kiongozi anachafuliwa jina bila msingi wowote na hizo huenda ziwe laana kwa wale walifanya uovu huo,” alisema Tamaro.