Katibu wa muungano wa walimu nchini Knut tawi la Kilindini mjini Mombasa Dan Aloo amemtaka waziri wa elimu Fred Matiangi kuhakikisha kuwa walimu waliousimamia mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne na darasa la nane mwaka uliopita wanalipwa marupurupu yao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Aloo, aliikashifu hatua ya baraza la mtihani nchini Knec kuchelewesha malipo hayo licha ya kandarasi ya walimu hao kueleza kuwa wanafaa kulipwa chini ya miezi minne baada ya kuusimamia mtihani huo.

‘’Hii ni kuwadhulumu walimu, hata sheria inasema kuwa mtu akishafanya kazi anafaa kulipwa. Hatua ya Knec kusalia kimya ilhali wanajua wana deni la walimu ni jambo linalodhihirisha kuwa hawako tayari kufanyi kazi na walimu wetu,’’ alisema Aloo.

Afisa huyo sasa anamtaka waziri wa elimu Fred Matiangi pamoja na kaimu mwenyekiti wa Knec Profesa George Magoha kuingilia kati swala hilo na kuhakikisha kuwa malipo hayo yanatekelezwa kabla ya shule haijafunguliwa kwa muhula wa pili lau sivyo watachukua hatua.

Kulingana na mwalimu mmoja aliyezungumza na mwandishi huyu kwa sharti la kutotajwa, walimu waliotahini na kusahihisha mtihani huo hawajapokea malipo yao huku juhudi zao za kuwasiliana na Knec zikikosa kufaulu hasa tangu baraza hilo livunjiliwe mbali kufuata tuhuma za wizi wa mtihani.