Jumla ya wamiliki 70 wa maduka ya kuuza dawa katika ukanda wa Pwani wametiwa nguvuni katika muda wa majuma mawili yaliyopita.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya maafisa wa bodi inayosimamia madawa nchini, kuidhinisha oparesheni kali dhidi ya wamiliki wanaohudumu kinyume cha sharia.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la Kisauni wakati wa oparesheni hiyo, afisa mkuu wa ukaguzi wa madawa katika bodi hiyo Julius Kaluai, alisema kwamba hatua hiyo iliafikiwa baada ya kubainika kwamba ni maduka elfu sita pekee ya kuuza dawa yaliyosajiliwa humu nchini, huku mengi zaidi yakiendeleza shughuli zake kinyume cha sheria.

Kaluai alisema wamiliki wengi wanaohudumu kwenye maduka hayo hawajahitimu, hali inayowasababisha wamiliki wa maduka hayo kutoyasajili.

“Watu kama hawa ndio wanahatarisha maisha ya wakaazi kwa kuwapatia dawa bila ufahamu wala maelezo yoyote kuhusiana na dawa hizo,” alisema Kaluai.

Afisa huyo alisema kuwa tayari waliokamatwa wameshtakiwa mahakamani na kutozwa faini.

Alisisitiza kwamba wahudumu hao wanapaswa kuhitimu katika taaluma hiyo kabla ya kumiliki maduka ya dawa humu nchini, pamoja na kusajili maduka yao katika bodi hiyo.

Oparesheni hiyo imekuwa ikiendelezwa katika Kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu, na itaanzishwa tena kabla ya mwisho wa mwaka huu kukamilika ili kuhakikisha kwamba maduka yaliyosajiliwa pekee na yanayohudumiwa na wataalam waliofuzu ndiyo yanayohusika katika maswala ya dawa nchini.