Wamiliki wa vilabu pamoja na hoteli katika kaunti ndogo ya Kangundo wameagizwa kujenga vyoo katika majengo yao ili kuwakidhi wateja wao.
Naibu wa kamishna wa kaunti ndogo ya Kangundo Samuel Njora alisema kuwa alitoa agizo hilo baada ya kugundua kuwa biashara nyingi hazina vyoo.
Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo hilo. Njora alisema kuwa ukosefu wa vyoo umechangia katika kuzorota kwa mazingira.
Aidha, Njora alielezea kufedheheshwa na namna watu hasa walevi hujisaidia katika nyuta za nyumba au kando ya barabara wanapotoka kwenye vilabu.
"Ukianzisha biashara hasa pale watu watakula na kunywa, hakikisha una vyoo visafi ili biashara yako iimarike zaidi,” alisema Njora.
Njora aliwapa wamiiki hao wa hoteli na vilabu notisi ya mwezi mmoja kuhakikisha wana vyoo visafi.
Alisema kuwa atakayekiuka agizo hilo atajipata mashakani.
Aliwaomba wamiliki hao kuwa msitari wa mbele kudumisha mazingira kwa kuhakikisha mahala pao pa kazi ni pasafi na kuasi kutupa taka ovyo.