Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi katika eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, wamesema kuwa bidhaa nyingi zinazouzwa kwenye maduka ya bidhaa kuukuu katika eneo hilo ni za wizi.

Akiongea siku ya Jumatatu mkuu wa polisi katika eneo la Kisauni Richard Ngatia alisema kuwa wanaendeleza msako katika maduka hayo ili kunasa bidhaa hizo.

Alisema kuwa baada ya bidhaa hizo kuibiwa kutoka kwa wananchi, hupelekwa katika maduka hayo na kisha kuuzwa tena kama bidhaa kuukuu.

“Huu ni mwanzo tu. Tutaenda katika kila duka hapa Kisauni na tutahitaji wenye hayo maduka kuthibitisha ni jinsi gani walivyopata bidhaa hizo,” alisema Ngatia.

Mkuu huyo wa polisi aliwalaumu wamiliki wa maduka hayo kwa kile alichokitaja kama kuchangia hali hiyo kwa kukubali kununua na kuuza mali ya wizi.

“Kwa vile wamiliki wa maduka hayo wanakubali kununua mali ya wizi, wao ndio wanaochangia wizi kuongezeka zaidi katika eneo hili,” aliongeza Ngatia.

Eneo la Kisauni kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na visa vya uhalifu huku vijana wadogo wakihusishwa na visa hivyo.