Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Muungano wa wamiliki wa matatu mjini Mombasa umeitaka Mamlaka ya usalama barabani NTSA, na maafisa wa trafiki kuzingatia sheria wanapotekeleza oparesheni ya kusaka magari mabovu barabarani.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa muungano wa Matatu Owners Association tawi la Mombasa, Sammy Gitau, alisema kuwa wanaunga mkono msako huo ila hawajaridhishwa na namna inavyotekelezwa.

Gitau alisema wamepata lalama nyingi kutoka kwa wahudumu wa magari mjini humo, hasa madereva wanaodai kuhangaishwa na baadhi ya maafisa wa NTSA na polisi wa trafiki.

“Tunaunga mkono msako dhidi ya magari mabovu barabarani lakini tuwe na utu. Isiwe kuwa hata wale wasio na hatia wanadhulumiwa. Wenye makosa wacha wachukuliwe hatua hata kama ni kuagizwa warekebishe makosa yao lakini tusiwakandimize wasio na hatia,” alisema Gitau.

Mamlaka ya usalama barabarani NTSA imekuwa ikitekeleza msako dhidi ya magari mabovu mjini Mombasa tangu mapema wiki hii, katika hatua inayolenga kuondoa magari yasiyofaa yakiwemo yale yasio na mikanda ya usalama na vithibiti mwendo.