Wahudumu wa bodaboda eneo la Kisimani eneo bunge la Nyali katika mtaa wa Freretown waliandamana kulalamikia mauaji ya hapo jana ya kijana aliyehusishwa kuwa mwanachama wa Wakali Kwanza.
Wahudumu hao walisema kuwa kijana huyo kwa jina Hamisi aliyepigwa risasi na maafisa wa usalama mapema jana hakuwa na uhusiano wowote na kundi hilo na kwamba huenda serikali ikawa imeshindwa kuwasaka wanachama wa wakali kwanza eneo hilo na kuwageukia wanabodaboda.
Wakiongea katika kituo cha kuegesha pikipiki cha uwanjani huko Freretown, wahudumu hao sasa wameitaka idara ya usalama haswa maafisa wa polisi wanaohudumu eneo hilo kuwa waangalifu zaidi wakati wanapowasaka wahalifu kwani sio wote wanaorandaranda ni wahusika wa kundi la wahalifu.
Aidha, wamesema kwamba iwapo idara ya usalama mjini Mombasa inataka kukabiliana na visa vya mara kwa mara vya utovu wa usalama eneo la Kisauni na Mombasa kwa ujumla basi ni sharti serikali ya kaunti ikishirikiana na serikali kuu kujenga vituo zaidi vya polisi kwani wanaotekeleza uhalifu sasa wamewajulia muda maafisa wa polisi.
Wahudumu hao aidha wamewaonya vijana wenzao wanaojihusisha na visa vya utovu wa usalama kwa kuwapora kina mama eneo hilo.