Wanabodaboda wa kituo cha Marani kilichoko wadi ya Marani eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti wamemwomba mwakilishi wao wa wadi kuwajengea kibanda cha kujikinga wakati huu wa mvua.
Wakiongea na mwanahabari huyu siku ya Jumanne asubuhi katika kituo chao, wanabodaboda hao walisema wanasumbuka wakati mvua inaponyesha, jambo ambalo limewapelekea kumwomba mwakilishi wa wadi hiyo Dennis Ombachi kuwajengea kibanda ambacho kitawasaidia mvua inaponyesha.
“Tunamwomba mwakilishi wetu atukumbuke atujengee kibanda maana tunasumbuka sana mvua inaponyesha,” alisema Nyakundi
“Mwakilishi wetu tayari amejenga vibanda kwingine, lakini eneo hili la Marani bado hajajenga kibanda, ikumbukwe kuwa Marani ni ngome ya wanabodaboda wote maana ndio kituo kikubwa,” aliongezea Nyakundi.
Wanabodaboda hao wamesema mvua inaponyesha, wengi wao huenda makwao ili kuepuka kunyeshewa.
“Mimi ninapoenda kwangu mvua inaponyesha, napata hasara kubwa maana mvua inapokamilika kunyesha, kurudi kwa kituo cha bodaboda wale wa karibu na kituo hicho tayari wamewasafirisha wateja, ndio maana tunahitaji kibanda sio cha kutusaidia wakati wa mvua bali hata wakati wa kiangazi kutokana na jua kali,” alisema Okinyi.
Wakati huo huo, wanabodaboda hao walimtaka mwakilishi huyo kuwaanzishia chama chao cha kupokea mikopo ili waweze kujiendeleza na kujimaarisha kimaisha
“Ikiwezekana mwakilishi wetu, atuanzishie chama cha kupokea mikopo kama sisi wanabodaboda, wengi wetu tunaendesha pikipiki za wenyewe lakini tukipata mikopo ianaeza tusaidia tununue pikipiki zetu,” alihoji Omambia.