Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana kutoka kaunti ya Kisii wametakiwa kuwa makini wanaponunua pikipiki, haswa kutoka kwa watu binafsi ili wasiingie kwa mitego ya uhalifu.

Wahudumu hao pia wameshauriwa kuhakikisha kuwa stakabadhi za piki piki husika zipo tayari kabla ya kufanya uamuzi wowote wa kununua.

Akiongea siku ya Alhamisi kwenye mahojiano ya na huyu mwandishi, mwenyekiti wa jumuia ya wanabodaboda katika kaunti ya Kisii Mike Mose alisema kuwa imekuwa vigumu visa kama hivyo kupungua, ikizingatiwa kuwa baadhi ya wezi ni majambazi hatari na wana ujuzi hata wa kugushi stakabadhi na kuuza pikipiki bila mnunuzi kujua.

Matamshi ya mwenyekiti huyo yanajiri siku tano tu baada ya msako wa polisi kupata zaidi ya pikipiki tano ambazo ziliibiwa kutoka kaunti ya Kisii kupatikana katika eneo la mpakani Kuria, ambapo alisema kuwa wengi wa waathiriwa huwa ni vijana ambao wameanza kuendesha pikipiki hivi karibuni na hawajakuwa na ujuzi na njia za kutambua walaghai ambao mara nyingi hujifanya mteja na kuwaibia.

Mose aliwashauri pia vijana wawe na makundi ili iwe rahisi kujipatia pikipiki mpya, kuliko kuendea zile ambazo zimetumika.

Aidha, aliwasihi kuwa iwapo watataka kununua pikipiki ambazo zimetumika, sharti wazinunue kutoka kwa mtu ambaye wanamfahamu ili kujiepusha na kununua mitambo za uwizi.