Share news tips with us here at Hivisasa

Wanabodaboda mjni Kisii wameunga mkono msako wa pombe haramu ambao unaendelea kutokana na walevi wengi kuwasumbua kwa kutowalipa wanapowabeba.

Wakiongea siku ya Alhamisi katika mtaa wa mwembe mjini Kisii wakati kijana mmoja mlevi alipoanguka kutoka juu ya pikipiki, wanabodaboda hao walitaja kuwa walevi wamekuwa na mazoea ya kuanguka huku wengine wakiruka kutoka juu ya pikipiki, na mara nyingi wao ndio hulaumiwa jambo likifanyika.

Kulingana na wanabodaboda hao, kijana huyo ambaye alikuwa amelewa alianza kumpiga mwanabodaboda aliyekuwa amembeba, jambo lililosababisha kuanguka kwake.

“Nilishtukia mtu akinipiga kofi kutoka kwa mgongo na wakati nilijaribu kumuulizia, ndiposa akanipiga zaidi nami nikajaribu kumkanya kwa kuwa tulikuwa kawa barabara lakini aliendelea na akaanguka,” alihoji mwanabodaboda aliyekuwa amembeba.

Kwa sasa wanabodaboda hao wamepongeza msako wa pombe haramu ambao unaendelea, na kusema kuwa walevi huwasumbua sana haswa wakati wamewabeba na kukataa kulipa, jambo ambalo huleta shida kubwa katika biashara zao.

“Mwenye pikipiki hawezi kuelewa kuwa haukupata pesa kwa sababu ulibeba walevi wakakata kutoa pesa, yeye kitu anahitaji ni pesa na sisi hubeba ili kuwasaidia lakini wao hawatusaidii,” alihoji Jim Momanyi, mwanabodaboda

Aidha, walikanusha madai ya wengi wanaosema kuwa wao ndio hutumiwa kusafirisha pombe kutoka maeneo mbalimbali.

“Kuna watu wengi wanaosema kuwa sisi ndio ushirikiana na wagema kusafirisha pombe, mimi kwa kweli pikipiki yangu haijawai beba pombe,” alihoji Geoffrey Mogeni.