Baada ya waziri wa masuala ya ardhi nchini Jacob Kaimenyi kuvunjilia mbali bodi za kuthibiti masuala ya ardhi kote nchini, sasa wanachama wa bodi hizo tawi la Nyamira wamejitokeza kulalamikia vikali hali hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na wanahabari siku ya Jumanne mjini Nyamira, wanachama hao zaidi ya kumi wakiongozwa na mshiriki wao Emmanuel Otero walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakihudumu kwenye bodi hizo bila kulipwa marupurupu yao. 

"Kwa muda wa miaka kumi tumekuwa tukiifanyia serikali kazi kwenye bodi za ardhi bila malipo na tungali tunadai pesa nyingi na tunashangazwa na sababu ya waziri wa ardhi kuvunja bodi za ardhi bila ya kutulipa marupurupu yetu kwanza," alisema Otero. 

Otero aidha alimtaka waziri Kaimenyi kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa wanachama wa bodi hiyo tawi la Nyamira wanalipwa marurupu yao ya zaidi ya shillingi millioni 2 kabla ya kuvunjilia mbali bodi hizo. 

"Tunashangazwa mbona waziri Kaimenyi avunjilie mbali bodi za ardhi nchini ilhali hatujalipwa marupurupu yetu na ndio sababu tunamrahi Kaimenyi kuhakikisha tumelipwa kabla ya kungatuka kwetu," aliongezea Otero.