Juhudi za kuwarai wanachama wa magenge ya uhalifu kujisalimisha kwa polisi zinaonekana kuzaa matunda baada ya vijana wanane kujisalimisha siku ya Jumatano.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri siku moja baada ya vijana 15 wa genge la 'Young thugs' kuandamana na wazee wa mitaa kujisalimisha kwa polisi.

Wanane hao, waliokuwa ni pamoja na wasichana watatu, ambao ni wanafunzi wa shule za upili, waliandamana na jamaa zao mpaka afisini mwa naibu kamishna wa Likoni Bwana Geoffrey Omoding.

Vijana hao waliapa kutohusika tena katika vitendo vya uhalifu.

Akizungumza baada ya kuwapokea vijana hao, Omoding alisema kuwa waliojisalimisha hawatachukuliwa hatua za kisheria.

"Bado kuna muda wa vijana zaidi kujisalimisha. Nawahakikishia kuwa watakaojisalimisha kwa hiari yao hawatochukuliwa hatua za kisheria,” alisema Omoding.

"Vijana wakiwa katika makundi haya ya ujangili huwa rahisi mno kujipata wameingia katika kundi la al-Shabaab. Nimeona ni heri kuwaleta mapema kabla ya kujipata mahali pabaya zaidi,” alisema mmoja wa wazazi aliyekuwa ameandamana na vijana hao.

Inaripotiwa kuwa vijana hao ni miongoni mwa wale ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakaazi katika eneo la Majengo Mapya, Likoni.