Mwanachama wa Jubilee Kaunti ya Mombasa Ali Mwatsahu akiwahutubia wanahabari hapo awali. Picha/ the-star.co.ke
Licha ya mgombea wa kiti cha ugavana Kaunti ya Mombasa Suleiman Shahbal na mgombea mwenza Ananiah Mwaboza kupatanishwa hivi majuzi, baadhi ya wanachama wa Jubilee wameonyesha kutoridhishwa na hatua hiyo.
Wanachama hao wamewataka viongozi wa Jubilee kuandaa kura za mchujo kwa kiti cha ugavana Kaunti ya Mombasa kwa kile walichokitaja kama ukosefu wa ushirikiano bora baina ya viongozi hao.
Wakiongozwa na Ali Mwatsahu, wanachama hao walisema kuwa imebainika wazi kwamba kuna utengano baina ya Shahabal na Mwaboza, hatua aliyoitaja kusababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwao.
Mwatsahu alisema kuwa hali hiyo huenda ikaleta mgawanyiko mkubwa katika chama hicho.
“Endapo swala hili halitachukuliwa kwa uzito basi huenda chama cha Jubilee kikakosa umaarufu Mombasa na hata kukokosa kunyakua viti mbalimbali vya uongozi ifikapo uchaguzi mkuu. Ningependa kuwahimiza viongozi wa chama hiki kukubaliana kufanya kura za mchujo,” alisema Mwatsahu.Wakati huo huo, Mwatsahu alisema kuwa uongozi bora huletwa na ushirikiano wala sio kubaguana kupitia misingi ya kisiasa.Aliongeza kuwa wako tayari kushirikiana na kiongozi yeyeyote atakayeshinda kwenye kura hizo ya mchujo.