Wanachama wa chama cha Kanu tawi la Mombasa, wamemtaka mwenyekiti wao wa kitaifa Gideon Moi, kujiuzulu na kuandaa uchaguzi wa maafisa wapya wa chama hicho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza kwenye kikao na wanahabari katika hoteli moja mjini Mombasa, wanachama hao, wakiongozwa na mwenyekiti wa tawi la Mombasa Harith Saleh Shahbal, wamesema kuwa ni lazima kufanyika kwa mabadiliko hayo.

Walimpa Moi makataa ya chini ya mwezi mmoja kuondoka ofisini, kabla ya kuchukua hatua za kumngo’a.

Vile vile, wamemtaka mwenyekiti huyo kutotumia jina la chama cha Kanu kugombana hadharani na Naibu Rais William Ruto, kwa kusema kuwa anachafua jina la chama hicho, kilichoheshimika kwa miaka mingi.

“Tunaomba mheshimiwa Gideon Moi ajiuzulu wadhfa wake na kuitisha uchaguzi katika chama kutokana na udhaifu wa uongozi,” alisema Harith.

Aidha, wamelitaka baraza kuu la kitaifa la chama hicho kusitisha shughuli za kuuza mali ya chama hicho kote nchini.

Wakati huo huo, wamesema kuwa wanatarajia kusimamisha wagombea wao katika nyadhfa zote za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao, ila huenda wakabadilisha nia hiyo iwapo watakubaliana vingine na vyama vinavyounga muungano ulioko serikalini.