Washukiwa wanne wa kundi la uhalifu la Wakali Kwanza wameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya kujiandaa kutekeleza uhalifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mohamed Abubakar pamoja na wengine watatu wanadaiwa kujiandaa kutekeleza visa vya uhalifu katika eneo la Mwembe Tayari, Kaunti ya Mombasa wakiwa wamejihami kwa silaha hatari.

Kiongozi wa mashtaka Erick Masila aliambia mahakama siku ya Jumatatu kuwa wanne hao wanadaiwa kuhusika na visa kadhaa vya uhalifu mjini Mombasa, na kusababisha usalama na uchumi kuzorota.

Masila alitaka mahakama kuwaachilia washukiwa hao kwa dhamana ya kiwango cha juu.

Wanne hao walikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Teresia Matheka, na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 50 kila mmoja.

Matheka pia ameagiza mshukiwa wa nne Swaleh Musa kupelekwa katika Hospitali kuu ya mkoa ya Pwani kubaini umri wake.