Wanachama wa kundi la MRC sasa wanaitaka mahakama kuwaondolea mashtaka ya kuwa wanachama wa kundi haramu.
Hatua hii inajiri baada ya mahakama kuu kuhalalisha kundi hilo na kulitaja kama kundi halali lisilo la kigaidi na haramu kama ilivyodaiwa.
Zaidi ya wanachama 20 wanaokabiliwa na madai hayo katika Mahakama ya Mombasa kupitia wakili wao Yusufu Abubakar, wameitaka mahakama kuwaachilia huru.
Siku ya Jumatatu, Wakili Abubakar aliambia mahakama kuwa kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu uhalali wa kundi hilo, basi ni sharti wateja wake waondolewe mashtaka yote yanayowakabili.
“Itakuwa vyema iwapo wateja wangu wataondolewa mashtaka yote yanayowakabili kwa sababu kundi la MRC sio haramu,” alisema Abubakar.
Hatua hii imeilazimu afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umaa kuomba kuahirishwa kwa kikao cha kesi hiyo kwa kusema kuwa haikuwa tayari kuiedesha siku ya Jumatatu.
Wanachama wengi wa MRC wanakabiliwa na kesi za kuwa wanachama wa kundi haramu.
Kesi hiyo itasikizwa tena Agosti 29, mwaka huu.