Wanachama wa kundi la MRC wametakiwa kujiandikisha kama wapiga kura huku zoezi la kusajili wapiga kura likiingia siku ya tatu.
Kauli hii imetolewa na naibu chansela wa Chuo kikuu cha Taita Taveta Hemed Boga, aliyewataka wanachama hao kujiandikisha kwa wingi ili kuwachagua viongozi bora watakaotetea maslahi yao.
Boga amewataka wafuasi hao wa MRC kuandikisha kundi hilo kama chama cha kisiasa, ili wapate fursa ya kuendeleza agenda yao kisheria bila ya kutumia njia za mkato.
“Itakuwa bora iwapo MRC itasajiliwa kama chama cha kisiasa ili kiweze kuwasilisha matakwa yao bungeni,” alisema Boga.
Kundi la MRC linatambulika kwa kauli yake ya 'Pwani si Kenya'.
Kundi hilo linadaiwa kujaribu kuvuruga uchaguzi wa 2013, na kusababisha maafa ya watu pamoja na baadhi ya maafisa wa usalama.