Wanachama wa ODM eneo bunge la Likoni wanamtaka mbunge wa eneo hilo Masoud Mwahima kuwasilisha barua ya kujiondoa kwake kwenye chama hicho baada ya kuasi kanuni za chama na kutangaza bayana kuwa atajiunga na JAP kwenye uchaguzi ujao.
Akizungumza kwenye kikao na wanahabari siku ya Jumapili katika afisi za chama hicho huko Likoni, mwenyekiti wa chama hicho Hamisi Ali Domoko, alisisitiza kuwa Mwahima anapaswa kijiuzulu kama mbunge wa eneo hilo ili uchaguzi mdogo ufanyike.
Domoko amemtaja Mwahima kama kiongozi asiyekuwa na msimamo thabiti baada ya kushawishiwa na Jubilee kukihama chama chake kilichompeleka bungeni.
Aidha, amesisitiza kuwa kulingana na sheria za taifa mwanasiasa yeyoto atakayeasi chama chake anapaswa kujiuzulu ili uchaguzi mdogo kufanyika.
Hatua hii inajiri baada Mwahima kuweka bayana kuwa atajiunga na JAP kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2017.
Katika uwanja wa Shika Adabu, siku ya Jumamosi, Mwahima alisema katika uchaguzi ujao eneo hilo litampigia kura Uhuru.