Katibu mkuu wa chama cha ODM Ababu Namwamba amesema malumbano baina ya viongozi wa chama cha ODM katika Kaunti ya Nyamira hayafai kushuhudiwa kwa kuwa yanaathiri mshikamano wa chama hicho mashinani.
Akizungumza katika Shule ya msingi ya Kenyamware alipomtembelea mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba Abuya Abuya, katibu huyo alisema kuwa badala ya viongozi kulumbana na kupiga siasa duni, yafaa waweke mikakati yakuhakikisha kuwa wanaiondoa mamlakani serikali ya Jubilee kwenye uchaguzi mkuu ujao.
"Badala ya viongozi wa ODM katika eneo hili kuendelea kulumbana hadharani nakupiga siasa duni, yafaa waweke mikakati yakuiondoa serikali iliyopo mamlakani ifikapo uchaguzi mkuu ujao," alisema Namwamba.
Namwamba aidha aliwasihi wanachama wa ODM kuwaheshimu viongozi waliochaguliwa na akawaomba kuwa imara na shupavu kwenye chama ili kukiimarisha chama hicho mbele ya uchaguzi mkuu ujao.
Katibu huyo aidha aliwaomba viongozi wa chama hicho kusuluhisha tofauti zao kwa njia mwafaka pasi na kuanika hadharani tofauti zao mbele ya umma.
"Kukubaliana na kutokubaliana miongoni mwa viongozi ni jambo la kawaida na hiyo ndiyo demokrasia, lakini hiyo sio ithibati tosha ya viongozi kulumbana hadharani," alisema Namwamba.
Haya yanajiri baada ya wabunge wa chama hicho katika Kaunti ya Nyamira wakiongoza na mbunge wa Mugirango Magharibi James Gesami na mwenzake wa Mugirango Kaskazini Charles Geni Kulalamikia uongozi wa mbunge wa kitutu Masaba Timothy Bosire ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ODM Nyamira na pia vilevile mweka hazina wa kitaifa wa chama hicho.