Jumla ya wanafunzi 32,733 waliofanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka huu kutoka ukanda wa Pwani watajiunga na shule za upili mwaka ujao.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mshirikishi mkuu wa elimu ukanda wa Pwani Dickson ole Keis alisema kwamba idadi hiyo ya wanafunzi imeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana.
Keis alisema kuwa wanafunzi 1,844 kutoka ukanda wa Pwani watajiunga na shule za kitaifa.
Aidha, alisema kwamba huenda zaidi ya wanafunzi elfu 15 kutoka ukanda wa Pwani wakakosa kujiunga na shule za upili kutokana na kukosa kufikisha alama zaidi ya 200.
Kaunti ya Mombasa na Kilifi ndizo zinazoongoza kwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na shule za upili mwaka ujao, huku idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa KCPE Pwani ikiwa ni 77,164.