Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baadhi ya wazazi na familia kadhaa mjini Mombasa wana furaha baada ya watoto wao kubahatika kupata ufadhili wa masomo kutoka kwa mpango wa Wings To Fly unaodhaminiwa na benki ya Equity.

Ingawaje takriban wanafunzi 147 waliofanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka jana katika kaunti hiyo walituma maombi, ni 60 ndio walioteuliwa kupata ufadhili huo, huku wengi wao wakisemekana kuwa wanatoka sehemu ya Likoni.

Mpango huo wa Wings to Fly huwafadhili wanafunzi werevu kutoka katika familia maskini nchini.

Bodi maalum hulazimika kutembelea familia husika kuhakikisha ikiwa kweli familia hizo zinapitia changamoto za maisha na kushindwa kugharamia karo.

Katika hafla iliyowaleta wanafunzi hao pamoja na wazazi wao mjini Mombasa siku ya Jumamosi, mwenyekiti wa bodi inayohusika kuwateua wanafunzi hao Bi Margaret Wandario alisema kuwa zoezi la uteuzi hupitia changamoto nyingi kwani wanafunzi wengi hutuma maombi na wote huwa wamefaulu vyema.

Hata hivyo, wazazi ambao watoto wao walifanikiwa kuteuliwa walieleza furaha yao huku wakisema kuwa mpango huo utawasaidia pakubwa kwani wengi wao ni maskini.

“Mimi nimeshukuru sana kwa sababu hata sikujua mwanangu atasoma vipi, lakini sasa amepata ufadhili na niko na imani atasoma bila shida,” alisema mzazi mmoja.

Katika mpango wa mwaka huu wa 2016, Wings To Fly ilipokea maombi 22,000 kote nchini lakini ni wanafunzi 2,000 waliopata nafasi hiyo.

Wanafunzi hao walisafiri siku ya Jumatatu hadi mjini Nairobi kwa semina maalum kabla ya kukongamana katika ukumbi wa Kasarani siku ya Ijumaa, ambapo Rais Uhuru Kenyatta pamoja na mkurugenzi mkuu wa Equity James Mwangi wanatarajiwa kufanya uzinduzi rasmi.