Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa wamekashifu vurugu zilizozuka katika Chuo Kikuu cha Nairobi siku chache zilizopita.
Chuo Kikuu cha Nairobi kimefungwa kwa muda usiojulikana, kufuatia uamuzi ulioafikiwa na bodi simamizi ya chuo hicho kutokana na rabsha za wanafunzi.
Rabsha hizo zilizuka baada ya baadhi ya wanafunzi kudai kuwa uchaguzi wa chuo hicho haukua halali, na kumtaka aliyeteuliwa kama mwenyekiti ya muungano wa wanafunzi Babu Owino kujiondoa.
Akizungumza siku ya Jumatano, kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa Mark Rigo alisema kuwa anakashifu vikali kitendo hicho na kusema kuwa viongozi wasitumie wanafunzi vibaya.
Aliongeza kuwa chuo hicho pia kinatarajiwa kuenda kwenye uchaguzi hivi karibuni na kuwaomba wanafunzi wenzake kutoleta vurugu la aina yoyote.
Chuo hicho pia kilikumbwa na vurugu hapo awali baada ya wanafunzi kuandamana kulalamikia kuongezwa kwa karo.