Wanafunzi wa vyuo vikuu mbali mbali katika Kaunti ya Mombasa wameitaka serikali kupeana fedha za matumizi kutoka kwa hazina ya mikopo ya vyuo vikuu nchini HELB ili kuwawezesha kuboresha maisha yao.
Wakiongozwa na katibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Pwani Francis Muthaura katika maandamano ya amani siku ya Jumatatu, wanafunzi hao walisema kuwa ukosefu wa pesa za matumizi husababisha wanafunzi kujiingiza kwenye makundi ya kigaidi na kuzorotesha maisha yao na jamii zao kwa jumla.
“Inabidi serikali itupatie fedha za matumizi ili wanafuzi wasiweze kushiriki katika makundi ya kigaidi kwa ukosefu wa fedha hizo,” alisema Muthaura.
Aidha, kiongozi wa Chuo Kikuu cha Moi tawi la Mombasa, Mohammed Kaimey, ameitaka serikali kushirikiana na wanafunzi ili kuhakikisha mipangilio ya muundo msingi imeboreshwa.
“Ni muhimu serikali kuhusisha wanafunzi wa vyuo vikuu katika miundo msingi ili kudumisha amani na kuongeza ajira nchini,” alisema Kaimey.
Vilevile, Mwakilishi wa kina mama Kaunti ya Mombasa, Mishi Mboko, ameitaka serikali na washikadau mbali mbali kushirikiana ili kueneza amani, na kupunguza kesi za vijana kujiunga na kundi la al-shabab miongoni mwa makundi mengine ya kigaidi.
“Ushirikiano na washikadau mbalimbali katika jamii utaimarisha uwepo wa vijana kutojihusisha na makundi ya kigaidi yakiwemo al-shabab,” alisema Mboko.”
Aidha, Mishi alisema kuwa ushirikiano huo utawezesha vijana kufahamu umuhimu wa matumizi bora ya mtandao ili kuweza kuboresha maisha yao na jamii kwa julma.
“Asili mia kubwa ya vijana haijapata ajira na ushirikiano katika jamii utawawezesha vijana kufahamu na kutotumia mitandao ya kijamii katika mipangilio ya kigaidi,” alisema Mboko.
Vile vile, Mboko alisema kuwa ukosefu wa amani utadororesha uchumi wa taifa katika sekta ya utalii na biashara zingine zinazohusisha mataifa ya nje.