Wanafunzi wawili wa chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa TUM wanaosomea uhandisi wamezindua ndege isiyo na rubani maarufu kama –drone.
Wanafunzi hao wanasema wamezindua ndege hiyo kwa madhumuni ya kufuatilia matukio ya kiusalama hapa nchini.
Simon Hinga na Irene Ndung’u wanasema visa vya utovu wa usalama nchini na mashambulio ya kigaidi vimewachochea wao kubuni kifaa hicho.
“Ukikumbuka matukio ya Westgate, na pia kule Kapedo ambapo polisi wetu wengi waliuawa kwa sababu ni sehemu zilizojaa milima na kama tungekuwa na kifaa kama hiki tungesaidika sana,” alisema Hinga.
Naye Irene anaongeza kuwa kifaa hicho kina kamera maalum inayoweza kunasa na kutuma picha kikiwa hewani.
“Hiyo kamera itakuwa inafuatilia mienendo ya watu na kutuma picha kwa tarakilishi zetu na pia itakuwa inasaidia pakubwa maafisa wa usalama kama kuna maadui katika mpaka,” aliongeza Ndung’u.
Wanafunzi hao sasa wanasema endapo kifaa hicho kitakubalika na idara ya usalama nchini kitasaidi kwa kiasi kikubwa kufuatilia na kuwanasa magaidi.