Wito umetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi, upili, taasisi za kiufundi na vyuo vikuu katika eneo la Pwani, kutia bidii masomoni ili kuboresha viwango vya elimu.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwazawadi wanafunzi waliofanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE mwaka jana, katika ukumbi wa Tononoka mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga alisema kuwa ni muhimu kwa wanafunzi kuzingatia masomo wakati wanapokuwa shuleni pamoja na kushirikiana na walimu wao ili kuinua viwango vya elimu vilivyokisiwa kudorora.
Gunga aliwataka wazazi kutembelea shule za watoto wao na kufahamu tabia na mienendo ya watoto wao hususan watoto wa kike ili kuwaepusha na mimba za mapema.
“Tafadhalini wanafunzi fanyeni kila juhudi shuleni kwa kutia bidii ili kuinua viwango vya elimu vilivyoshuka. Hatua hiyo itaeleta mabadiliko makubwa katika eneo hili la Pwani katika siku za usoni,” alisema Gunga.