Wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Gusii (GUsii Institute of Technology) wamevunja na kupora mali ya kituo cha mafuta cha Tosha kilichoko mkabala na chuo hicho.
Rabsha hizo zilitokea baada ya wanafunzi wawili na wafanyikazi wawili wa taasisi hiyo kugongwa na kuawa papo hapo na gari lililokuwa limebeba miti ya stima katika barabara kuu ya kutoka Kisii kuelekea Keroka siku ya Alhamisi jioni ambapo waliifunga barabara hiyo na kuwalazimu wenye magari na pikipiki kutumia barabara tofauti.
Kulingana mwanafunzi mmoja wa Chuo hicho Jones Karebwa, ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa gari hilo ambaye inadaiwa alikuwa Polisi, kupoteza mwelekeo na kuwagonga wanne hao ambao walikuwa wakielekea nyumbani baada ya shughuli ya siku.
Polisi ambao waliwasili eneo hilo la mkasa kudhibiti hali hiyo walijipata pabaya baada ya wanafunzi ambao walikuwa na hasira kuwazidi nguvu na kufurusha Maafisa hao wa Polisi.
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi pale wanafunzi hao walilichoma gari hilo ambalo lilisababisha ajali na baadaye kugeukia kituo cha mafuta cha Tosha na kuvunja huku wakipora kwa ushirikiano na wapita njia walionekana wamebeba mitungi ya gesi, kreti za soda, viti na bidhaa nyinginezo ambazo waliweza kufikia.
Maafisa wa Polisi walikuwa wametumwa wengi kupambana na wanafunzi hao wenye walisababisha rabsha katika barabara hilo huku miili za waliofariki kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti Kisii.