Polisi mjini Naivasha wamewatia mbaroni watoto wawili wa shule, katika eneo la Mai Mahiu ambao wamekuwa wakiishi pamoja kama mume na mke baada ya kutoroka shuleni.
Wawili hao walitiwa mbaroni siku ya Jumatatu baada ya kutafutwa kwa muda na maafisa wa idara ya upelelezi kupitia kwa simu zao.
Msichana huyo akona na umri wa miaka 14 na alikuwa katika darasa la sita, naye kijana ana umri wa miaka 18 kutoka shule moja ya upili ya eneo hilo.
Wakazi wa eneo la Mai Mahiu walifurika kwa wingi katika nyumba walimokuwa wakiishi wawili hao, kabla ya polisi kuwaondoa na kuwapeleka katika kituo cha polisi cha Naivasha kwa mahojiano zaidi.
Mkaazi mmoja, Jane Muthoni, alisema msichana huyo alitoroka nyumbani kwao eneo la Site, mjini Naivasha mwezi jana, na juhudi za kumtafuta zilipo gonga mwamba, wakawaarifu polisi walioanza kumtafuta kupitia kwa simu ya kijana huyo.
OCPD wa Naivasha Titus Munyoki, alidhibitisha tukio hilo na kusema wawili hao wamepelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu.
Munyoki alisema kuwa iwapo matokeo ya matibabu yatabaini kuwa wawili hao wameshiriki ngono, kijana huyo atafikishwa mahakamani na kushtakiwa na ubakaji.