Kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, wanafunzi wasichana wapatao mia tatu wa shule ya msingi ya Ekenyoro, wadi ya Bonyamatuta wamekosa pahala pa kujisaidia baada ya vioo vyaokuporomoka na kuzama.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Ijumaa mwalimu mkuu wa shule hiyo Peter Ombogo, vyoo hivyo viliporomoka wakati wanafunzi wote walikuwa wamerejea makwao kutoka shuleni na ni bahati hamna mwanafunzi yeyote aliumia.
"Ni bahati kwamba hamna mwanafunzi yeyote aliyeumia kutokana na kuporomoka na kuzama kwa vyoo kwa maana wakati wa tukio hilo wanafunzi wote walikuwa manyumbani, ila hofu yangu ni kwamba huenda shule hii ikafungwa na maafisa wa afya ya umma kutokana na hali hii," alisema Ombogo.
Aidha, Ombogo alisema kwa hivi sasa wanafunzi hao wasichana wamepewa choo kimoja cha wavulana kutumia ikizingatiwa kuwa shule hiyo iko na wanafunzi zaidi ya mia sita.
"Kwa sababu kwamba hatutaki shughuli za masomo ya wanafunzi shuleni kuathirika kutokana na hali hii, tumetenga choo kimoja cha wavulana ili kitumiwe na wasichana huku tukingoja wasamaria wema watusaidie," aliongezea Ombogo.