Wanafunzi wa Shule ya Upili ya walio na changamoto ya kusikia ya Ngala walifanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi wa shule hiyo siku ya Ijumaa.
Uchaguzi huo ulioongozwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ulikuwa wa kuchagua viongozi kama vile kiranja mkuu, naibu wa kiranja mkuu, kiranja wa chumba cha maankuli, kiranja wa chumba cha burudani pamoja na kiranja wa michezo ambapo Daniel Mwangi aliibuka kama kiranja mkuu.
Kwenye hotuba yake kupitia kwa mtafsiri, Mwangi aliwashukuru wanafunzi wa shule hiyo kwa kumpigia kura huku akiwaahidi kwamba atatimiza ahadi aliyowapa ya kuboresha mawasiliano kati yao na walimu miongoni mwa ahadi zingine.
Naye mwakilishi wa walio na ulemavu katika bunge la Kaunti ya Nakuru Emma Mbugua ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria uchaguzi huo, alishukuru tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kwa kuunga mkono walio na ulemavu katika uchaguzi wao, kwa kusimamia uchaguzi huo.
Alisema kuwa uchaguzi huo unaonyesha wazi kwamba walio na ulemavu wana uwezo sawia na wale wasiokuwa na ulemavu.
Katika uchaguzi huo, Ahmed Hassan aliibuka mshindi kwenye nafasi ya naibu wa kiranja mkuu, huku Emmanuel Muuo akipata nafasi ya kiranja wa burudani.
Wengine waliochaguliwa kwenye nafasi ya uongozi ni William Kariuki aliyeibuka kama mshindi kwenye nafasi ya kiranja wa bweni la wavulana na Mitchell Akinyi aliyechaguliwa kama kiranja wa bweni la wasichana.