Kwa mara ya kwanza wanafunzi katika fani ya uhandisi wamejumuishwa katika hafla ya kufuzu kwa mahafala katika chuo cha kiufindi cha Mombasa (TUM).

Share news tips with us here at Hivisasa

Kaimu mhadhiri mkuu wa chuo hicho Profesa Laila Abubakar amesema kwamba baada ya vuta ni kuvute kati ya bodi kuu ya uhandisi nchini na chuo hicho, bodi hiyo imehakiki taaluma hiyo inayofunzwa katika chuo hicho cha TUM.

Hii ni baada ya wanafunzi wa chuo hicho kuzuiliwa kufuzu ikisemekana kwamba masomo waliyokuwa wakipewa chuoni humo hayakuwa yametimiza viwango hitajika vya ubora kulingana na bodi hiyo.

Abubakar alisema kuwa hapo awali, wanafunzi waliyokamilisha masomo yao ya uhandisi katika chuo hicho walilazimika kujisajili na chuo kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta ili kufuzu kama wahandisi, jambo lililochangia migomo ya mara kwa mara na uharibifu wa mali chuoni humo.

“Ilikuwa changamoto kuu kukabiliana na migomo ya mara kwa mara kutokana na hali ya wanafunzi kushindwa kufuzu katika fani ya uhandisi ila kwa sasa hali hiyo imetanzuliwa,” alisema Abubakar.

Profesa Abubakar alisema kwamba jumla ya wanafunzi 79 waliokuwa wamesomea taaluma hiyo ya uhandisi na kufuzu katika viwango vya stashahada na shahada ya shahada na ambao walifika mahakamani kuushtaki usimamizi wa chuo hicho sasa wamefurahishwa na hatua ya kuhakikiwa kwa mafunzo hayo.

Alisema kuwa wanafunzi hao wako tayari kabisa kuiondoa kesi hiyo mahakamani.

Jumla ya wanafunzi 2, 334 wamefuzu chuoni humo katika taaluma mbali mbali, huku 268 wakifuzu katika fani ya uhandisi katika viwango vya stashahada na shahada.