Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kisii wanahadaiwa mboga na wafanyibiashara. Hii ni kutokana na kiangazi ambacho kimekumba eneo hilo tangu Januari na hivyo kupelekea kukosekana kwa mboga za majani haswa sukuma wiki.
Ili kukidhi mahitaji ya wateja wao, wafanyi biashara hao wamebuni njia mbadala. Kweli nyani akikosa nyama hula nyasi.
Wamekua wakichukua maganda ya mboga aina ya drum head ambayo yana rangi ya kijani kibichi na kuchanganya na sukuma wiki. Hivi hua vigumu kutambua tofauti uliopo. Mwanafuzi mmoja ambaye alihadaiwa alieleza kuwa alishangaa jinsi mboga hizi zilikuwa gumu hata baada ya kupika kwa muda.
“Niligutushwa baada ya kupika mboga hizo nikifikiria ni sukumawiki kumbe ilikuwa ni hadaa,” alieleza wakati wa mahojiano.
Hili ni janga linalowakabili wanafunzi wengi kwani mboga hapo zamani zimekua zikiuzwa kuanzia Sh5, lakini kwa sasa mboga chini ya shilingi kumi na tano haitoshi mtu mmoja na kwa sasa wanalazimika kununua ya angalau Sh20.
Ni jambo la kushangaza kwani eneo la Kisii linasifika kwa uwezo wake wa kukuza mboga za kila aina kutokana na hali nzuri ya anga.
Baadhi ya wanafunzi wanalazimika kununua samaki aina ya omena ili kuepuka hadaa za wafanyibiashara hawa. Wanafunzi hao kwa sasa wanawaomba wafanyi biashara hao kuwa makini kwani huenda wakapoteza wateja wao wa kila siku.
Lakini mmoja wa wafanyi biashara hao, Mama Moraa, alieleza kuwa kiangazi ndicho kimewalazimu kuanza kuchanganya mboga japo yeye bado hajamhadaa yeyote.
“Hali ya anga ndio kisababishi japo si tabia nzuri katika biashara,” alieleza Mama Moraa.
Wanafunzi wamesisitiza ya kuwa ni lazima tabia hiyo potovu ikome na isahaulike katika kaburi la sahau au watagoma kununua mboga kwa wafanyabiashara hao.