Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wa chuo cha ufundi cha Mombasa sasa wanamshtumu Mwakilishi wa Wadi ya Portreitz Fadhili Mwalimu kutokana na mswada wake wa kutaka wanafunzi wa chuo hicho kugharamia hasara ya magari mawili ya taka waliyoteketeza mapema wiki hii.

Kulingana na kiongozi wa muungano wa wanafunzi wa chuo hicho Ocharo Ondiek, magari hayo yaliteketezwa na watoto wa kuranda randa mitaani na wala sio wanafunzi wa chuo hicho.

Ondiek alimkosoa mwakilishi huyo wa wadi akisema kwamba anajitafutia umaarufu wa kisiasa na kwamba hajafanya uchunguzi wowote kabla ya kuwasilisha mswada huo katika bunge la Kaunti.

“Tunasikitishwa na Mwakilishi wa Wadi ya Portreiz Fadhili Mwalimu kwa hatua aliyoichukua ya kuwasilisha mswada katika bunge la kaunti kuwa wanafunzi tulipe gharama za magari ya taka, sisi hatujachoma magari. Tunamuomba afanye uchunguzi wa kina kabla ya kuwasilisha mswada katika bunge hilo,” alisema Ondiek.

Hatau ya kuchomwa kwa magari hayo ya taka mapema wiki jana imechangia kufutiliwa mbali kwa msaada wa karo na vifaa vingine kwa wanafunzi hao kutoka kwa gavana wa kaunti hiyo ya Mombasa Hassan Ali Joho.

Ondiek alimtaka Gavana Joho kufutilia mbali kauli yake ya kuwanyima wanafunzi hao usaidizi wa kielimu kutoka kwa serikali hiyo ya kaunti akisema kwamba watataabika.

“Tunamuomba Gavana wetu Hassan Ali Joho kufutilia mbali kauli yake ya kutunyima usaidizi kwani wanafunzi wa chuo hiki wanahitaji sana usaidizi wake,” aliongeza Ondiek.

Hata hivyo, Mwalimu aliutetea mswada wake na kusema kwamba wanafunzi hao wameisababishia serikali ya kaunti ya Mombasa hasara kubwa na ni lazima bunge la Kaunti hiyo libuni sheria ya kuwaadhibu.