Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wote wa shule mbalimbali nchini wameombwa kutodanganywa na baadhi ya vikundi kujihusisha na mambo ya uhalifu.

Akizungumza siku ya Jumapili katika mji wa Kisii, askofu wa Barokia ya Kakamega Joseph Obanyi aliwaomba wanafunzi kutia bidii kwa masomo ili waje kujisaidia siku za usoni kupitia masomo yao.

Aliwaomba wanafunzi kutojihusisha na masuala ya uhalifu nchini ili kupata riziki huku akisema uhalifu utaadhiri maisha yao.

“Nawaomba wanafunzi msidanganywe na yeyote kuwa ukijiunga na mambo ya uhalifu na kuwauwa wakenya wenzenu mtaenda mbinguni. Hayo ni mambo ya udanganyifu,” alisema askofu Obanyi.

Wakati huo huo, askofu huyo aliwaomba walimu kushirikiana na wazazi kuelimisha wanafunzi jinsi wanastahili kuishi katika ulimwengu huu na kutojihusisha na masuala ya ualifu nchini.

Walimu pia waliombwa kutia motisha wanapowafunza watoto ili waweze kupita katika mitihani yao ya kitaifa na kufurahia matunda ya walimu wao.

“Walimu wanapowasaidia wanafunzi kupita katika mitihani, wanafunzi hao huwa wanawakumbuka katika siku za usoni. Nawaomba mtie bidii ili viwango vya masomo viinuke zaidi katika sehemu zote za nchi,” aliongeza Obanyi.

Wakaazi wa eneo hilo waliunga mkono matamshi ya askofu huyo huku wengi wakisema wanafunzi hudanganywa kutumia dawa za kulevya na baadaye kujiingiza katika maswala ya uhalifu.

“Tunaomba walimu wa shule zote kujaribu wawezalo kuhakikisha wanafunzi hawatumii dawa za kulevya maana imebainika kuwa utumizi wa dawa hizo huchangia kujiunga na masuala ya ualifu,” alihoji Evans Ochako, mkaazi.