Mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kisii Profesa John Akama amewahimiza wanafunzi kutumia talanta zao ili kijinufaisha maishani.
Akiongea kwenye hafla ya kampeni dhidi ya dawa za kulevya siku ya Ijumaa kweye uwanja wa michezo wa Chuo hicho, Profesa Akama aliwapa wanafunzi hao wosia murwa huku akiwapa kongole waandalizi wa hafla hiyo.
“Hii ni fursa nzuri kwa vijana wakakamavu kukuza talanta zao na kuajibika kimaisha na kimasomo,” alisema Profesa Akama.
Aliongezea kuwa ni Kongamano kama hizo ambazo zitawafaa vijana kwa kumaliza utangamano na kuleta umoja na kukuza maadili mema miongoni mwa vijana katika jamii.
Iwapo vijana watajitumbukiza katika lindi la utumizi wa dawa za kulevya, basi huenda wakajiletea madhara kadha wa kadha ikiwemo wizi, magonjwa ya zinaa na kutotimiza mazimio yao maishani kama ipasavyo.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na kikundi cha wanaskauti kutoka Chuo Kikuu cha Kisii na kudhaminiwa na kampuni ya Vinywaji ya Coca-Cola, ilileta pamoja takribani Shule kumi kutoka Jimbo la Kisii. Baadhi ya Shule zilizoshiriki ni Shule ya Upili ya Daraja Mbili, Shule ya Kitaifa ya Kisii, Nyabururu miongoni mwa zingine.
Michezo walioshiriki ni kama mbio za mita 100, 800, na 1,200. Mchezo wa handiboli na kuruka pia hazikuachwa nyuma.
Wanafunzi walioshiriki wamewashukuru waandalizi kwa kuwapa fursa ya kuelimika kuhusu madhara ya utumizi wa dawa za kulevya.