Shule ya muda iliyokuwa imeanzishwa na wanafunzi, chini ya mti, katika eneo bunge la Lari imefungwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya waalimu kushurutishwa na korti kurejea darasani jumatatu wiki ijayo.

Shule hiyo iliyokuwa na takribani wanafunzi, 50 ilianzishwa punde tu mgomo wa waalimu ulipong’oa nanga wiki mbili zilizopita.

Wanafunzi hawa kutoka shule mbalimbali katika eneo bunge la Lari walikuwa wanakutana kila asubuhi kando na maduka ya Nyambari na kusoma kwa pamoja chini ya mti mmoja.

Watoto hawa walikuwa wameletwa pamoja na wanafunzi wawili, Geoffrey Matu na Partick Waweru amabo walimaliza masomo yao ya kidato cha nne mwaka uliopita.

“Ninajua umuhimu wa masomo na ndiyo sababu nilifanya bidii kuwasaidia watoto hawa waalimu wao walipo goma,” asema Waweru.

Kulingana na wasomi hawa moja ya changamoto walizopatana nazo ni miale ya jua kali pamoja na kelele kutoka kwa magari na wapita njia.

Kitendo hiki cha watoto hawa kiliwavutia wengi ambao walisema kuwa, walikuwa watoto wenye nidhamu na wenye hamu ya masomo.

Mzazi mmoja, Pauline Njihia alisema kuwa alifurahi kwani mtoto wake aliungana na wengine na kusoma badala ya kucheza tu na kupoteza muda.

Mwandishi mkuu wa chama cha waalimu, KNUT, tawi la Kiambu Magharibi Michael Muna alidhibiti kuwa walimu watarudi shuleni siku ya Juamtatu kama korti ilivyoamuru.