Hali ya huzuni ilitanda katika eneo la Nyang’oma katika Kaunti ya Kisumu, siku ya Jumanne, baada ya wanafunzi watano wa Shule ya chekechea ya AIC Awasi kuaga dunia papo hapo, baada ya kugongwa na gari katika barabara kuu ya Ahero-Awasi.
Watoto hao walikua kando ya barabara hiyo walipogongwa na gari dogo aina ya Toyota Saloon.
Akidhibitisha kisa hicho, OCPD wa Nyando Elias Gitonga, alisema kuwa dereva wa gari hilo alipoteza mwelekeo alipokua akijaribu kukwepa kuwagonga wanafunzi wengine wawili waliokua katikati ya barabara.
Watoto hao wawili walipata majeraha mabaya na wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga jijini Kisumu.
“Gari hilo lilikua likiendeshwa kwa mwendo wa kasi sana na dereva akokosa mwelekeo alipojaribu kukwepa kuwagonga wanafunzi waliokuwa wakivuka barabara,” alisema Gitonga.