Wanafunzi waliohitimu masomo yao ya shule ya upili wamewataka viongozi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinaimarishwa katika eneo la Pwani.
Wakizungumza siku ya Ijumaa, wanafunzi hao walisisitiza kuwa fedha za ustawishaji wa maeneo bunge zinastahili kutumika katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu.
Kulingana na Philip charo, aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya upili ya St George's kaloloeni, wanafunzi wengi wanaofukuzwa shule kwa misingi ya ukosefu wa karo huwa ndio wanaosoma kwa bidii zaidi ikilinganishwa na wale wasio na matatizo yoyote ya kifedha nyumbani.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga aliwataka viongozi wenzake kutambua kuwa katika kila jamii kuna wanafunzi ambao huwa wanahitaji misaada mbalimbali katika kuafikia safari yao ya elimu katika maisha yao.
Gunga ambaye alikuwa mgeni wa heshima na mwanzilishi wa mradi wa kuwasimamia wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kujilipia karo, alizitaka serikali za kaunti haswa katika eneo la Pwani kuungana kuanzisha mfumo wa kuwafadhili wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia karo.
“Nawahakikishia wanafunzi na walimu kuwa tutatumia fedha za ustawi wa maeneo bunge kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga madarasa, mabweni na hata kuwalipia baadhi ya wanafunzi karo, ili kuhakikisha kuwa viwango vya elimu katika eneo la Pwani vinaimarika,” alisema Gunga.
Wanafunzi hao aidha wametoa wito kwa wabunge katika eneo la Pwani kuungana kuwasaidia wanafunzi wote pasi kuwabagua kwa misingi ya dini wala familia.