Wanafunzi werevu kutoka jamii maskini katika Kaunti ya Kisumu watanufaika na mradi wa Elimu Kwa Wote baada ya shirika moja lisilo la Kiserikali kuzuru eneo hilo.
Elewana Non-Governmental Organisation (ENGO) lililo na makao yake nchini Marekani limezuru Kaunti ya Kisumu na sasa linaendesha kampeni za kuhamazisha wananchi katika Kaunti hiyo kuhusu umuhimu wake.
Kampeni hizo zinaongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu, Zaky Mcesaz iliyezuru Shule ya St. James Sinyolo ilioko katika Kata ya Sinyolo Wilaya ya Maseno mnamo siku ya Ijumaa, wakati alipodokezea walimu na wazazi kuhusu faida za shirika lake katika eneo hilo na humu nchini kwa jumla.
Mcesaz alihoji kuwa shirika lake linawasadia wanafunzi werevu kutoka jamii maskini kwa kuwalipia karo wanapoingia kwenye shule za upili na kusimamiwa kimasomo hadi kwenye Vyuo Vikuu na hata kuajiriwa kazi baada ya masomo. Alisema kuwa wanafunzi watakaopata alama za uastani kwenye mtihani wao ndio watakaofaidika na mradi huo.
“Shirika letu linalenga masomo tu. Tunahakikisha kuwa wanafunzi werevu ambao wazazi wao hawajiwezi kifedha wanapata kutimiza ndoto yao kwa kumaliza masomo yao,” alisema Mcesaz.
Aidha kiongozi huyo wa shirika alidokeza kuwa ni lazima wanafunzi hao kujisajili na Sh1,000 kabla ya majina yao kuingizwa kwenye orodha ya watakaofaidika kwa kulipiwa karo.
Shirika hilo lilizuru humu nchini mnamo mwaka 2008, wakati lilipoanzisha kazi yake katika Magharibi mwa Kenya, likianzia kule Teso Kusini katika Kaunti ya Busia na kuenea katika Bungoma na Kakamega. Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa wanalenga kuzifikia kaunti zote nchini ifikapo mwaka 2030.