Shirika la kutetea haki za binadamu la National Citizen Engagement Forum NACEF limeshutumu baadhi ya vyombo vya habari Kwa kuegemea mirengo ya siasa.
Mwenyekiti wa shirika hilo lenye makao Nakuru, Moses Gitonga katika mahojiano ya kipekee afisini mwake, alisema kuwa baadhi ya wanahabari wameanza kuwa wafisadi na kuegemea upande mmoja wa siasa.
Kwa mujibu wake, baadhi ya wanasiasa wanawalipa wanahabari ili kutochapisha taarifa mbaya dhidi yao.
"Tunajua vizuri baadhi ya wanasiasa ambao wanatumia fedha nyingi kuhitilafiana na utendakazi wa vyombo vya habari humu nchini," Gitonga alisema.
Alidai kuwa baada ya wanahabari kulipwa, baadhi ya taarifa hukosa kutokea katika vyombo vya habari.
"Mwanahabari anafanya taarifa ya ujasusi kuhusu mwanasiasa kisha mwanasiasa huyo anapotambua anatafuta mwanahabari huyo na kumlipa fedha kisha taarifa hiyo inapotea" Gitonga alisema.
Aliongeza kuwa huo ni ufisadi wa hali ya juu na wanahabari wanafaa kumakinika na kutekeleza wajibu wso bila kuingiliwa na mtu yeyote.