Mwanaharakati wa haki za binadamu Masese Kemunche ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kujali maslahi ya wanahabari. Masese, ambaye pia ni mratibu wa mipango katika shirika la Centre for Enhancing Democracy and Good Governance-CEDGG, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba wanahabari wanapitia masaibu chini ya waajiri wao ilhali wamiliki wa vyombo vya habari wanazidi kutengeza faida.
"Vyombo vya habari vinazidi kuwahangaisha wanahabari ilhali wanatekeleza wajibu mkuu katika vituo hivyo," Masese alisema.
Mwanaharakati huyo alisema kuwa wanahabari wengi wa vituo vya redio mjini Nakuru wanateseka kutokana na mishahara mibaya ilhali wao hufanya kazi muhimu ya kuifahamisha jamii.
Alisema kuwa amepata lalama kadhaa kutoka kwa wanahabari wanaohudumu katika vituo vya radio wanaohangaishwa na waajiri wao huku wengine wakikosa kulipwa hata mshahara.
Ni kutokana na hilo ambapo alitoa wito kwa wanahabari kutonyamaza wakati wanapoteswa na wamiliki wa vyombo vya habari. "Wanahabari ni wa maana sana na hawafai kuhangaishwa inapofika mahala pa mshahara," Masese alisema.