Shirika moja la haki za binadamu linalopigania uwazi na uwajibikaji limeomba wanahabari kuchunguza visa vya matumizi mabaya ya pesa za umma serikalini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa shirika la Stand for Human Rights Daniel Makori, alisema kuwa serikali, hasa zile za kaunti ndizo hutumia pesa za umma vibaya kutokana na kutokuwepo kwa upinzani mkali kwenye mabunge ya kaunti.

Makori alidai kuwa wawakilishi wa wadi huhongwa ili kutofichua matumizi mabaya ya pesa serikalini.

"Vyombo vya habari ndivyo vinavyoweza kutegemewa kutoa habari za matumizi mabaya ya pesa za umma serikalini kwa kuwa baadhi ya wawakilishi wadi hushawishika kuficha habari za matumizi mabaya ya pesa za umma," alisema Makori.

Makori aidha alishangazwa na hali ya visa vya ufisadi kugatuliwa kutoka serikali kuu hadi kwenye serikali za kaunti, akiongeza kuwa umma na vyombo vya habari tu ndivyo vinavyoweza kutegemewa kusimamia ukweli kuhusiana na visa vya ufisadi.

Wakati huo huo, Makori alimpongeza aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi nchini Anne Waiguru kwa kuamua kujiuzulu.

"Ni jambo lakushangaza kwamba ufisadi unaendelea kukithiri katika idara nyingi za serikali ya kaunti. Hali hiyo inaibua maswali ya iwapo ufisadi ndio uliogatuliwa kutoka kwenye serikali kuu badala ya huduma muhimu kama za afya. Hata hivyo, namshukru aliyekuwa Waziri wa Mipango ya kitaifa na Ugatuzi Anne Waiguru kwa hatua yake yakuamua kujiuzulu na kungoja uchunguzi kufanyika dhidi yake,” alisema Makori.