Mwenyekiti wa chama cha utalii katika ukanda wa Pwani Mohammed Hersi ametoa wito kwa waandishi wa habari kuripoti habari zenye manufaa kwa kaunti za Pwani.
Hersi aliwataka wanahabari kuasi tabia ya kuripoti habari za ugaidi na utumizi wa mihadarati.
Akizungumza baada ya mkutano na wakuu wa Wizara ya Utalii nchini siku ya Jumatatu, Hersi alisema kuwa matangazo kama hayo yanaathiri sekta ya utalii nchini.
“Mara nyingi habari ambazo huchapishwa kwenye vyombo vya habari huwa kuhusu mambo mabaya ambayo yanafanyika nchini, hivyo basi kuwafanya wageni kuogopa kuzuru humu nchini,” alisema Hersi.
Aidha, mwenyekiti huyo alitoa changamoto kwa serikali kuu na ile ya kaunti kutoa mabango yote ya kutangaza washukiwa wa ugaidi, kwa kusema kuwa haionyeshi ishara nzuri ya nchi.