Vyombo wa habari nchini hususan katika ukanda wa Pwani vimeonywa dhidi ya kupeperusha habari zinazolenga kuzua rabsha na machafuko hasa wakati huu ambapo taifa linaelekea katika mchakato wa kampeni za kisiasa.
Naibu Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini CA kanda ya Pwani, Joseph Kamunge, amesema kuwa mamlaka hiyo inafuatilia kwa kina vyombo vyote vya habari nchini na katika eneo la Pwani kuhakikisha kuwa matangazo yote yanayopeperusha hayakiuki sheria za nchini na uwanahabari.
Akiongea baada ya kongamano la wadau wa sekta ya uwanahabari katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Kamunge alisema kuwa iwapo vyombo vya habari vitazingatia swala hilo, basi kwa kiwango kikubwa taifa hili litakuwa la amani.
"Tunaviomba sana vyombo vya habari kuhakikisha kuwa vinakuwa na uangalifu hasa kuepukana na matangazo ama habari zinazoeneza chuki, na ambazo zinawezakuleta machafuko nchini, ili taifa hili liwe na amani,” alisema Kamunge.
Aidha, aliwaonya Wakenya wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza jumbe za chuki kuwa maafisa wa usalama watawachukulia hatua za kisheria, kwani hatua hiyo ni ukiukaji wa utumizi wa mitandao.
Mamlaka hiyo kwa sasa inazuru mashinani kuwahamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kutumia jumbe za amani na kudumisha usalama.