Wanahabari wa Mombasa.[Osman Suleiman]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanahabari jijini Mombasa wamezuiliwa kufuatilia na kushuhudia zoezi la kuhesabiwa upya kura za eneo bunge la Changamwe.

Wanahabari hao wamepatwa na mshangao baada ya maafisa wa tume ya uchaguzi kusema kuwa wamepewa agizo la mahakama kuwazuia wanahabari dhidi ya kushuhudia zoezi hilo ambalo linafanyika katika kituo cha kuhesabia kura katika jumba la  Public works eneo la Shimanzi.

Wanahabari hao wakiongozwa na Samir Ali kutoka Radio Rahma wamekashifu hatua na kuitaja kama ukiukaji wa haki za wanahabari.

Akizungumza siku ya Alhamisi, baada ya kuzuiliwa mwanahabari Samir amewataka wakuu wa vyombo vya habari pamoja na vyama vya kutetea wanahabari kuingilia kati ili kuona kwamba haki za wanahabari hazikiukwi.

Wanahabari wengine waliozuiliwa ni Galgalo Bocha wa gazeti la Nation, Malemba Mkongo wa gazeti la The Star pamoja na wanahabari wengine kutoka media max, Baraka fm na idhaa zingine.

Maafisa wa Iebc walioko katika kituo hicho wanadai kuwa kuna agizo lilitolewa na mahakama kuu ya Mombasa la kuwataka waandishi kutofuatilia zoezi hilo.

Hata hivyo Maafisa hao wameshindwa kuonyesha agizo hilo la Mahakama jambo ambalo linaibua wasiwasi miongoni mwa waandishi kuwa huenda maafisa hao wanajaribu kuwafunga macho kuficha mambo fulani.