Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeshutumu vikali hatua ya makundi ya kihalifu na ugaidi kutumia mavazi ya kidini kutekeleza uhalifu.
Shirika hilo limesema kuwa hatua kali za kisheria zinafaa kuchukuliwa dhidi ya wahalifu hao.
Akizungumza Kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumatatu, afisa wa maswala ya jinsia na haki za watoto katika shirika hilo, Salma Hemed, alisema kuwa hatua hiyo kamwe hailingani na dini ya Kiislam, ama dini yoyote ile.
Hemed alisema kuwa kuwa hatua hiyo inafaa kudhibitiwa mara moja na idara ya usalama.
Amewahimiza wakaazi kutoa taarifa za washukiwa wa ugaidi na wahalifu, ili kuwawezesha maafisa wa polisi kuwatia nguvuni, pamoja na kuimarisha usalama wa eneo nzima la Pwani.
Aidha, amesema kuwa tayari mashirika ya kijamii na yale yasiyo kuwa ya kiserikali yanashirikiana na idara za usalama eneo hilo kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa na wakaazi wanaishi kwa amani.
"Tunakashifu vikali hatua ya magaidi na wahalifu kutumia vazi la dini kujificha wanapoenda kutekeleza uhalifu. Tunawaomba wakaazi kutoa ripoti kwa maafisa wa usalama ili watu hao wakamtwa,” alisema Hemed.