Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu hapa Pwani wametaka kuundwa jopo huru litakalochunguza mauaji ya kiholela yanayoendelea kushuhudiwa humu nchini.
Katika kikao cha pamoja na mbunge wa Mvita Abdulswammad Nassir na seneta wa Mombasa Hassan Omar, wanaharakati hao wameeleza wasiwasi wao kuhusiana na kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara pamoja na mauaji ya kiholela yanayoaminika kutekelezwa na maafisa wa polisi.
Wakiongozwa na wakili Yusuf Abubakar katika kikao na wanahabari siku ya Jumapili, wanaharakati hao walitoa wito wa kuundwa jopo hilo huru wakisema hawana imani na uchunguzi unaondeshwa na maafisa wa polisi haswa baada ya wao kudaiwa kuwa wahusika wakuu wa mauaji hayo na utekanyaji nyara.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mvita Abdulswammad Nassir, alikashifu mbinu zinazotumika na maafisa wa polisi katika vita dhidi ya ugaidi, akisema kuwa mbinu hizo zimechangia uhasama mkubwa katika jamii bila ya polisi kutimiza lengo lao.
Abdulswammad alisema licha ya kutiwa mbaroni watu wanaoshukiwa kuwa magaidi na kisha baadaye kuwapata bila ya hatia, polisi hawajawajibika kuomba msamaha kwa waathiriwa kwa kuwachafulia majina.
Wakati huo huo seneta wa Mombasa Hassan Omar ameeleza kuwa sheria za kimataifa za uhalifu dhidi ya binadamu zinatoa mwongozo wa kufunguliwa mashtaka wale wote waliohusika ama kuchangia katika uhalifu huo wa kibinadamu ikiwemo wakuu wa polisi waliohudumu serikalini katika nyakati zilizopita.
Haya yanajiri huku takwimu kutoka tume ya kitaifa ya utetezi wa haki za binadamu zikionyesha kuwa jumla ya visa 125 vya watu kupotea kwa njia ya kuktananisha vimeripotiwa katika mwaka 2014-15 ambapo 81 kati yao hawajulikani walipo kufikia sasa.